Jeromu
Jeromu au Yeronimo (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) alikuwa mmonaki, padri na mtaalamu wa Biblia, aliyemudu vizuri lugha zote za kitabu hicho pamoja na Kilatini hata akawa mwandishi bora wa lugha hiyo kati ya mababu wa Kanisa.
Ujuzi wake huo mkubwa alioupata hasa Roma aliposoma na kubatizwa, ulimwezesha kutafsiri na kufafanua Biblia vizuri sana.
Kisha kupatwa na mvuto mkubwa kwa maisha ya sala, alishika juhudi, akahamia Mashariki ya Kati, akapadirishwa.
Aliporudi Roma, akawa katibu wa Papa Damaso I, halafu akahamia moja kwa moja Bethlehemu wa Yuda kuishi kimonaki. Hata hivyo aliendelea kujihusisha na mahitaji mbalimbali ya Kanisa hadi kifo chake uzeeni[1].
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Sikukuu yake inaadhimishwa tarehe 30 Septemba[2].
Maisha
haririAlizaliwa mwaka 347 huko Strido, sehemu za Dalmatia.
Alisomea hata Roma miaka ya 360 - 367, akijipatia elimu ya hali ya juu, aliyoiendeleza maisha yake yote, pia kwa safari nyingi magharibi na mashariki zilizomwezesha kufahamiana na watu wengi maarufu.
Katika ujana alivutiwa na maisha ya kidunia, lakini mvuto wa Ukristo ulishinda. Maisha yake yote alijilaumu sana kwa makosa yake ya ujanani, akazidi kutambua jinsi mtazamo wa Kipagani unavyopingana na maisha ya Kikristo.
Alibatizwa huko Roma akiwa na umri wa miaka 19, akaenda Aquileia kujiunga na jumuia ya askofu Valeriani akaendelea moja kwa moja kupambana kiume na tabia yake ngumu iliyochanganya ukali na wepesi wa kulia machozi, unyofu na elekeo la kinyongo, maisha magumu na hisia kali, uadilifu na hamaki, hisani na uchungu wa maneno.
Miaka 375 - 377 akiishi kama mkaa pweke katika jangwa la Kalchis, kusini kwa Alepo, Siria, pamoja na kunaliki vitabu, aliendeleza ujuzi wake wa Kigiriki na kuanza kufundishwa Kiebrania na Myahudi aliyeongokea Ukristo.
Mwaka 379, kisha kupewa upadri na askofu Paulino wa Antiokia alikwenda Konstantinopoli alipokamilisha ujuzi wake wa lugha ya Kigiriki chini ya Gregori wa Nazianzo.
Baada ya kuishi kama mmonaki miaka 3 akarudi Roma (382) na kuanza kutafsiri vitabu vya Origene, mpaka alipoteuliwa na Papa Damaso I kuwa karani na mshauri wake kutokana na sifa aliyokuwanayo kama mtawa na msomi.
Wakati huo alikamilisha ujuzi wake wa Kiebrania kwa msaada wa mwalimu wa dini ya Kiyahudi, na baada yake akazidi kutegemea elimu ya Kibiblia ya dini hiyo badala ya mbinu za Origene.
Akishika kazi, saumu, sala na makesha, alivuta wengi kumfuata Kristo kwa karibu zaidi hasa wanawake wa koo bora za Roma waliojifunza pia Kigiriki na Kiebrania ili wazidi kuelewa na kutekeleza Neno la Mungu chini yake.
Ndiyo sababu alikataa vitabu vya Deuterokanoni.
Baada ya Papa huyo kufa (385), upinzani dhidi yake mjini ulizidi, hivyo akahamia Mashariki ya Kati, ambapo alihiji Nchi Takatifu na kutembelea wamonaki wa Misri.
Hatimaye alianzisha na kuongoza monasteri kadhaa za kike na za kiume zenye elimu ya hali ya juu, akaishi katika mojawapo huko Bethlehemu, kuanzia mwaka 386 mpaka kufa kwake, akitafsiri na kufafanua Biblia hadi dakika yake ya mwisho (420).
Mafundisho yake
haririAlimuandikia Mt. Paulino wa Nola mwongozo wa maisha yake: “Jitahidi kujua duniani kweli zile zitakazodumu milele mbinguni… Je, tangu hapa duniani mtu hajisikii kukaa katika ufalme wa mbinguni anapoishi na maandiko hayo, anapoyatafakari bila kujua wala kutafuta kingine chochote?”
Aliandika pia, “Mtu angewezaje kuishi bila kujua Maandiko, ambayo kwa njia yake anajifunza kumfahamu Kristo mwenyewe, aliye uzima wa waamini?” Kwa njia ya Biblia “Mungu anasema kila siku na waamini”. “Ukisali, unasema na Bwanaarusi; ukisoma, ni yeye anayesema nawe”.
Alimuandikia padri Neposyani: “Soma mara nyingi Maandiko ya Kimungu; tena, afadhali mikono yako isitue kamwe Kitabu kitakatifu. Jifunze humo unachotakiwa kufundisha… Usibandukane hata kidogo na mafundisho ya mapokeo uliyofundishwa, hivi kwamba uweze kuhubiri kadiri ya imani sahihi na kupinga wanaoikanusha… Matendo yako yasiachane kamwe na maneno yako, isije ikatokea kwamba unapohubiri kanisani mtu aweze kujisemea, ‘Mbona basi mwenyewe hafanyi hivyo?’ Angewezaje kujadili mfungo mwalimu aliyeshiba? Hata mwizi anaweza kulaumu uroho; lakini katika padri wa Kristo, akili na maneno vinatakiwa kulingana”.
Pia aliandika kwamba kila mmoja anatakiwa kuwa na ushirika na “ukulu wa Mt. Petro. Najua kwamba Kanisa linajengwa juu ya mwamba huo”. “Mimi nipo pamoja na yeyote aliyeunganika na mafundisho ya Mt. Petro”.
Pamoja na hayo, “katika ufafanuzi wa Maandiko matakatifu tunahitaji daima msaada wa Roho Mtakatifu”.
“Tumpende Yesu Kristo, tukilenga daima kuungana naye: hapo hata yaliyo magumu yataonekana rahisi kwetu”.
Kuhusu makanisa, aliandika: “Inafaa nini kupamba kuta kwa vito ikiwa Kristo anakufa kwa njaa katika nafsi ya fukara?” Tena, “Tumvike Kristo katika fukara, tumtembelee katika mtu anayeteseka, tumlishe katika mtu mwenye njaa, tumkaribishe katika yule asiye na nyumba”.
Alimshauri hivi mama mmoja kuhusu malezi ya binti yake: “Hakikisha kwamba kila siku asome sehemu fulani ya Maandiko… Baada ya sala, lifuate somo, na baada ya somo, ifuate sala… Badala ya vito na mavazi ya hariri, apende Vitabu vya Kimungu… Kumbuka kwamba utaweza kumlea kwa mfano wako kuliko kwa maneno”.
Mashauri yake mengine yalikuwa haya: “Uyapende Maandiko matakatifu, na hekima itakupenda wewe; uyapende kwa dhati, nayo yatakulinda; uyaheshimu, nayo yatakubembeleza. Yawe kwako kama ushanga wako na hereni zako”. “Upende elimu ya Maandiko, nawe hutapenda tamaa za mwili”.
'Vulgata'
haririVulgata, tafsiri ya kwanza ya Biblia ya Kikristo nzima katika Kilatini ndiyo kazi yake muhimu zaidi. Aliianza kwa agizo la papa Damaso I mwaka 382, akaiendeleza kwa miaka 23. Tafsiri hiyo ilipitishwa rasmi na mtaguso wa Trento kwa tamko la kuwa haipotoshi kamwe imani, nayo ilitumika kama msingi wa tafsiri nyingine nyingi hadi karne XX, ikiathiri sana ustaarabu wote wa Magharibi. Hata hivyo tangu mwanzo ilikosolewa sana kwa kufuata mno msimamo wa Uyahudi. Ndiyo sababu Jeromu alitaka kukataa vitabu vya Deuterokanoni.
Maandishi mengine
haririPia alitafsiri vitabu vingine, alitunga hotuba, barua pamoja na vitabu juu ya maisha ya Wakristo watunzi maarufu zaidi ya 100 (yeye akiwa mmojawao) na ya wamonaki mbalimbali, akilinganisha safari zao za kiroho na vitabu vya kutetea imani kwa kupinga mafundisho ya wazushi.
Vilevile alihimiza wamonaki kuelekea ukamilifu, akafundisha vijana elimu ya kiutu na ya Kikristo na kupokea katika hoteli maalumu waliohiji Nchi Takatifu ili wasikose mapokezi kama ilivyowatokea Yosefu na Bikira Maria.
Sala yake
haririEe Bwana, umetupatia Neno lako kama nuru ambayo iangazie njia yetu; utujalie tulitafakari Neno lako na kufuata mafundisho yake hivi kwamba tuone hiyo nuru inazidi kuangaza hadi adhuhuri, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Tazama pia
haririTanbihi
haririVyanzo
hariri- J.N.D. Kelly, "Jerome: His Life, Writings, and Controversies" (Peabody, MA 1998)
- S. Rebenich, "Jerome" (London and New York, 2002)
Viungo vya nje
hariri- "St. Jerome" by Louis Saltet, in The Catholic Encyclopedia (1910)
- Jewish Encyclopedia: Jerome
- St. Jerome - Catholic Online
- The Story of St. Jerome and the Lion Ilihifadhiwa 12 Oktoba 2006 kwenye Wayback Machine.
- St Jerome (Hieronymus) of Stridonium Orthodox synaxarion
Maandishi kwa Kilatini
hariri- Maandishi yake yote katika Patrologia Latina ya Migne pamoja na faharasa
- Chronological list of Jerome's Works with modern editions and translations cited
- Opera Omnia (Maandishi Yote) from Migne edition (Patrologia Latina, 1844-1855) with analytical indexes, almost complete online edition
Google Books' Facsimiles
hariri- Migne volume 23 part 1 (1883 edition)
- Migne volume 23 part 2 (1883 edition)
- Migne volume 24 (1845 edition)
- Migne volume 25 part 1 (1884 edition)
- Migne volume 25 part 2 (1884 edition)
- Migne volume 28 (1890 edition?)
- Migne volume 30 (1865 edition)
Tafsiri za Kiingereza
hariri- English translations of Biblical Prefaces, Commentary on Daniel, Chronicle, and Letter 120 (tertullian.org)
- Jerome's Letter to Pope Damasus: Preface to the Gospels
- English translation of Jerome's De Viris Illustribus
- The Perpetual Virginity of Blessed Mary
- Lives of Famous Men (CCEL)
- Apology Against Rufinus (CCEL)
- Letters, The Life of Paulus the First Hermit, The Life of S. Hilarion, The Life of Malchus, the Captive Monk, The Dialogue Against the Luciferians, The Perpetual Virginity of Blessed Mary, Against Jovinianus, Against Vigilantius, To Pammachius against John of Jerusalem, Against the Pelagians, Prefaces (CCEL)