Charles Dickens
Charles Dickens (7 Februari 1812 – 9 Juni 1870) alikuwa mwandishi wa riwaya nchini Uingereza. Aliandika mengi na hadithi pamoja na riwaya zake zimetafsiriwa katika lugha nyingi.
Alizaliwa Landport-Portsmouth kama mtoto wa pili kati ya wanane. Alipokuwa na umri wa miaka 10 babake alifungwa gerezani kwa sababu ya madeni na mama pamoja na kaka na dada zake walihamia gerezani palepale. Charles pekee alibaki nje akaanza kutafuta kazi ili apate kulisha familia.
Pamoja na watoto wengine alifanya kazi katika ghala. Alipokuwa na miaka 12 aliendelea na kazi ya kiwandani akashindwa kusoma shule mara kwa mara.
Baada ya baba kuachishwa gerezani mwaka 1824 Vharles alipata nafasi ya kusoma na tangu 1827 akaajiriwa na wakili kama mtumishi wa ofisi. Hakuridhika na kazi hii akajifundisha hati mkato akaendelea kuwa karani bungeni na tangu 1831 alipata kazi kama mwandishi wa magazeti. Hapa alianza mwaka 1836 kutoa sura za riwaya yake ya kwanza iliyoitwa "The Pickwick Papers"; kila mwezi sura mpya ilichapishwa kama daftari na kuuzwa. Riwaya hii iliunda sifa yake kama mwandishi mashuhuri.
1837 aliendelea na riwaya "Oliver Twist". Mwishowe alikuwa mhariri wa magazeti makubwa akiendelea kutoa masimulizi na riwaya. 1865 aliathiriwa na ajali ya treni ambamo hakujeruhiwa kimwili bali ndoto za ajli ziliendelea kumtesa hadi mwisho wa maisha yake. 1868 alinunua nyumba kubwa ya kikabaila ya Gadshill Place iliyokuwa mahali pa kukutana kwa wasanii na waandishi. 1870 Charles Dickens aliaga dunia kwake nyumbani Gadshill. Alipewa kaburi kwenye kitengo cha washairi katika kanisa la Westminster Abbey.
Kazi zake
[hariri | hariri chanzo]Dickens kwa riwaya zake alijitahidi kuwakumbusha matajiri wa Uingerzea kuhusu hali ya watu maskini waliodharauliwa tu. Aliweza kutumia maarifa ya maisha yake kwa sababu aliwahi kuona mwenyewe jinsi gani haliy a umaskini na kuwa na madeni inaweza kuharibu maisha na maadili ya watu na jinsi gani wale waliobahatika katika maisha walivyowadharau wengine waliokosa bahati hasa watoto waliopaswa kuishi barabarani bila familia.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Charles Dickens mobile ebooks Ilihifadhiwa 27 Septemba 2007 kwenye Wayback Machine.
Makala hii kuhusu mwandishi fulani bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Charles Dickens kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |
- Charles Dickens Hakkinda Ilihifadhiwa 9 Februari 2012 kwenye Wayback Machine.